WEKA VIFAA HIVI KWENYE BANDA LA KUKU WAKO...


 

Ufugaji wenye tija unahitaji kuhakikisha kuwa vifaa muhimu vinakuwemo ndani ya banda kwa uwiano unaotakiwa kati ya kuku na vifaa hivyo. Vifaa hivyo ni pamoja na: 

a) Vyombo vya Chakula 

b) Vyombo vya Maji Viota

c) Vichanja, na 

d) Matandiko

a) Vyombo vya Chakula:

Ni muhimu kuwa na vyombo vya kutosha ili kuwawezesha kuku kula pasipo kusongamana. Vyombo hivyo lazima viwe safi na bora ili kuongeza ufanisi katika kufuga kuku

Vyombo vinavyotakiwa ni vile vinavyoweza kuzuia upotevu wa chakula. Kuku wasipewe nafasi ya kuchakura ndani ya vyombo hivyo ili kupunguza kupotea kwa chakula. Unaweza kuzuia upotevu huo kwa kuweka vyombo hivyo juu ya mawe, gogo au kuvining’iniza. 

Vyombo vya chakula vinaweza kutengenezwa na mfugaji mwenyewe kwa kutumia vifaa mbali mbali vilivyomo katika mazingira yake na si lazima vile vilivyotengenezwa viwandani. Baadhi ya vitu vinavyoweza kutumika ni pamoja na kipande cha gurudumu la gari lililotumika, gogo lililochimbwa kati na kadhalika.

Faida za kutumia vyombo bora:

-Huzuia kuchafuka kwa chakula

-Huzuia kupotea kwa chakula.

-Hupunguza uwezekano wa kuku kuambukizwa magonjwa kama vile coccidiosis, minyoo n.k.

b) Vyombo Vya Maji:

Vyombo vya maji ni muhimu sana kwa kuku pasipo kuangalia wanafugwa kwa mtindo gani. Maji safi ni muhimu sana kwa kuku kwani huwafanya kuku kuwa na afya bora na kuongeza ufanisi katika utagaji wa mayai. Ni vyema kutumia vyombo vya maji ambavyo ni rahisi kuvifanyia usafi, visivyo na uwezekano wa kumwaga maji hovyo. 

Vyombo vya maji ni vyema vikaning’inizwa ili kuwawezesha kuku kunywa maji kwa urahisi na pia kuzuia maji kuchafuliwa na kumwagwa kwa urahisi

c) Viota:

Ni vyema kuwepo na sehemu maalumu ya kutagia ndani ya banda la kuku. Sehemu hii inatakiwa kuwa tulivu, faragha na yenye mwanga hafifu,kutokuwepo kwa viota husababisha kuku kutaga mayai hovyo na kupotea kwa mayai mengi pasipo kujua na uanguaji huwa mbaya, hivyo kupunguza uzalishaji wa kuku na kurudisha nyuma shughuli ya uzalishaji.

kiota kinatakiwa kuwa na nafasi nzuri ya kumuwezesha kuku kuenea na kuweza kujigeuza. Kwa wastani kiota kinatakiwa kuwa na urefu wa sentimita 35, upana wa sentimita 35 na kina cha sentimita 35. Pia kiota kiwekwe juu kwa sentimita 50 toka sakafuni ili kumfanya kuku kujisikia salama zaidi.

Viota vinatakiwa viandaliwe mapema kulingana na idadi ya makoo uliyo nayo. Ndani ya kila kiota utatakiwa kuweka matandiko ili kuongeza joto na usalama wa mayai. Idadi ya viota iwe robo tatu ya idadi ya kuku waliofikia umri wa kutaga. 

d) Vichanja vya Kupumzikia na Kulala:

Kwa asili kuku hupendelea zaidi kulala juu kama kwenye miti kwani hujisikia kuwa na usalama zaidi kuliko wakiwa katika sehemu isiyo na mahali pa kudanda. Hivyo ili kuwafanya kuku wajisikie vizuri hapana budi kuwatengenezea vichanja sehemu ya nje wanaposhinda na kula chakula, na pia ndani ya banda ili kuwawezesha kulala vizuri nyakati za usiku.

kwa kawaida vichanja vinatakiwa vitengenezwe kwa urefu wa mita moja toka ardhini. Vijiti vya juu vyapaswa kuwa vya duara vyenye kipenyo kinachowezesha miguu ya kuku kuzunguka vizuri na kubana.

Faida za kutumia vichanja

-Huzuia kuku kulala hovyo ndani ya viota. Hupunguza mashambulizi ya wadudu kama viroboto, utitiri -na wadudu wengineo wanaoweza kuwa kwenye matandiko.

e) Uwekaji wa Matandiko: Matandiko yanaweza kuwa ni maranda ya mbao, makapi ya mpunga na kahawa n.k. Matandiko husaidia sana kufyonza unyevunyevu toka ardhini na kutoka kwenye kinyesi. Pia huzuia maradhi yatokanayo na baridi na unyevunyevu hususani kwa vifaranga. Utahitaji matandiko yenye ujazo wa unene wa sentimeta 5 hadi 10 ili kuwawezesha kuku wako kuwa katika hali iliyo nzuri. Mara unapoona dalili za matandiko kulowa inabidi kuyaondoa mara moja kwani ni rahisi kuoza na kuleta madhara kwa kuku. Inashauriwa kubadili matandiko ndani ya banda la kuku kila inapobidi.

Post a Comment

Previous Post Next Post