UNAE FUGA KUKU WA KIENYEJI FANYA HIVI...

 


MUHIMU KWA WAFUGAJI WA KUKU WA KIENYEJI/KUKU WANAO ATAMIA 

Kwa kawaida kuku wa Asili anapofikia umri kati ya miezi sita hadi minane huanza kutoa mlio (kutetea) unaoashiria yuko karibu kuanza kutaga mayai. Hivyo ni vyema viota viandaliwe mapema kuku wakiwa na umri wa miezi minne au mitano ili waanze kuvizoea.

Kuku anapoanza kutaga, akifikisha mayai matatu, mfugaji anashauriwa kuondoa kila yai linalozidi na kuacha hayo hayo matatu kila siku.Hakikisha kila yai linalokusanywa linawekwa alama ya tarehe au namba kwa kutumia kalamu ya risasi au penseli ili kumfanya kuku aendelee kutaga kwa lengo la kufikisha mayai 15 – 20. Mayai yanayoondolewa yahifadhiwe kwenye chombo kikavu chenye kupitisha hewa kama trei au boksi lililowekwa mchanga au hata chungu kilichojazwa mchanga. 

Fuata utaratibu ufuatao kuhifadhi mayai:

-Sehemu ya yai iliyochongoka iwe chini na pana iwe juu

-Hifadhi sehemu yenye kupitisha hewa ya kutosha na isiyokuwa na joto. 

-Mayai yasikae kwenye hifadhi hiyo zaidi ya wiki mbili toka siku yalipotagwa.

Sifa za mayai ya kuatamiwa

Ni vizuri kuchagua mayai ya kuatamia ili mayai yasiyofaa yaweze kuuzwa au kutumika nyumbani kwa chakula. Sifa za mayai mazuri ya kuatamiwa ni kama ifuatavyo:

1.Yawe masafi na wala yasisafishwe au kufutwa na kitambaa chenye maji kama ni machafu. 

2.Yasiwe na nyufa.

3. Yatokane na kuku aliyepandwa na jogoo. 

4. Yawe na ukubwa wa wastani kulingana na umbile au aina ya kuku. 

5. Yasiwe ya mviringo kama mpira pia yasiwe na ncha kali. 

6. Yasiwe yamekaa muda mrefu zaidi ya wiki mbili toka siku yalipotagwa. 

7. Yasiwe yaliyohifadhiwa kwenye sehemu yenye joto. 

Njia za uatamiaji na uanguaji:

Kuna njia mbili za uatamiaji na uanguaji, ambazo ni:

-Uatamiaji na uanguaji wa kubuni. 

-Uatamiaji na uanguaji wa asili.

Njia yoyote utakayochagua inahitaji maandalizi ya kina, hususani ya uchambuzi wa mayai yatakayoweza kutotolewa. 

Uanguaji wa Kubuni

Uanguaji wa kubuni ni kwamba mashine za kutotoleshea vifaranga (incubators) hutumika kuangua mayai mengi kwa wakati mmoja. Wafugaji wadogowadogo huwa na mashine za kutotolea vifaranga ambavyo huweza kuangua kati ya mayai 50 na 500. Mashine zinazotumika kutotoleshea vifaranga vya kuku wa kisasa zinaweza pia kutumika kutotoleshea vifaranga vya kuku wa kienyeji, aidha zipo mashine zinazotengenezwa hapa nchini na nje ya nchi.

Faida za kutumia mashine kutotoleshea vifaranga:

1.Vifaranga huanguliwa kwa wingi na wakati mmoja 

2. Vifaranga waliototolewa wakati mmoja hukua kwa pamoja na kuweza kuuzwa pamoja, hivyo hurahisisha uzalishaji. 

3. Kuku walionyang’anywa mayai ili yaanguliwe kwa mashine huanza kutaga tena mayai mapema hivyo hutaga mayai mengi kwa mwaka.

Changamoto za utumiaji wa mashine za kutotoleshea vifaranga:

1. Utaalam wa kutumia mashine huhitajika. 

2. Muda mwingi hutumika kufuatilia mwenendo wa mashine. 

3. Nishati ya uhakika huhitajika ama sivyo utotoaji hautakuwa mzuri.

Uanguaji wa asili:

Uanguaji wa asili ndiyo unaotumika kwa kuku wetu wa Asili ambapo kuku hutaga mayai na baadaye huatamia na hatimaye kutotoa vifaranga. Inashauriwa kumuwekea kuku mayai ya kuatamia kati ya 12 na 15 kwa wakati mmoja kufuatana na umbile la kuku.

Faida za uanguaji wa Asili wa vifaranga:

1. Gharama huwa ni kidogo. 

2. Mfugaji hahitaji ujuzi maalumu katika kufanya shughuli hii. 

3. Huhitaji kurekebisha joto, unyevunyevu, hali ya hewa na hata kugeuza mayai kama inavyofanyika kwenye mashine. 

4. Kutohitaji nguvu kazi yoyote.

Kuchagua mtetea anayeweza kuatamia mayai yasiyokuwa yake: Yaweza kutokea baadhi ya kuku wakawa watagaji wazuri wa mayai lakini hawapendi kuatamia. Katika hali hiyo ni vyema wakachaguliwa kuku (mitetea) wengine ili kuatamia mayai yao kwa uanguaji mzuri.

Utaratibu ufuatao utatumika

-Tafuta mtetea aliyefikia umri wa kutaga au kuku aliyekwishawahi kutotoa. 

-Tafuta mawe matatu ya mviringo au viazi mbatata vya ukubwa wa yai au vibao vilivyochongwa kwa umbile la yai (mayai bandia). 

-Muwekee kuku huyo mayai bandia yasiyopungua matatu kwenye kiota wakati wa usiku na umfungie humo usiku kucha hadi asubuhi na ukimuona anaendelea kuatamia basi usiku unaofuata toa mayai bandia na umuwekee mayai halisi. 

-Weka mayai kwenye kiota huku mikono yako ikiwa imepakwa majivu ili kuepuka kuwa na harufu kwani kuku anaweza kuyasusa.

Kuwatayarisha kuku wa kuatamia:

Kuku wanaotazamiwa kuatamia ni lazima wachunguzwe kwa makini kabla ya kuatamia ili kuhakikisha kwamba hawana chawa, utitiri au viroboto. Kuwepo kwa wadudu hao kutawafanya kuku wakose raha na wasitulie kwenye viota vyao, matokeo yake ni kuanguliwa kwa vifaranga wachache. Ili kuua au kuzuia wadudu hawa, fanya yafuatayo:

-Toa matandiko (litter) ndani ya kiota. 

-Nyunyiza dawa ya kuua wadudu (viroboto, utitiri nk.) ndani ya kiota.

-Pia mnyunyizie dawa kuku anayetarajiwa kuatamia

Kuwafanya kuku wengi kutotoa kwa wakati mmoja: 

Kuna uwezekano mkubwa tu wa kuweza kuwandaa kuku na kuweza kutotoa kwa siku moja. Njia ni rahisi na inaweza kuongeza tija katika ufugaji wa kuku wa Asili. Ili uweze kutotolesha kuku kwa wakati mmoja fanya yafuatayo:

Kuku anapotaga kila siku weka alama kila yai linalotagwa aidha namba au tarehe kulingana na siku aliyotaga. 

Yanapofika mayai matatu yaondoe na muwekee mayai bandia na huku ukiendelea kukusanya na kuweka alama mayai yanayoendelea kutagwa kila siku. 

Mara kuku anapoanza kuatamia unaweza kumuongezea mayai bandia na kufikia 8 hadi10. 

Fanya hivyo kwa kila kuku anayetaga hadi utakapopata idadi inayoweza kukupatia vifaranga wengi kwa wakati mmoja. Chagua mayai ya kuatamia ukianza na yai la mwisho kutagwa. 

Wawekee kuku wote mayai siku moja kwa kuondoa mayai bandia na kuwawekea mayai ya kweli wakati wa usiku. Kuku huendelea kuatamia mpaka vifaranga vitoke hivyo ukimwekea mayai yasiyo na mbegu, atakaa hapo hapo kwa muda mrefu. Kwa kawaida kuku huatamia mayai kwa muda wa siku 21 kabla ya vifaranga kuanguliwa.

Zoezi hili linawezekana iwapo uleaji wa vifaranga kwa njia ya kubuni litatumika kwani kuku mmoja anaweza kutotoa zaidi ya mara 7 kwa mwaka. Mafanikio ya mpango huu hupatikana kwa kuwanyang’anya kuku vifaranga vyao pale tu vinapototolewa (siku ya kwanza), na baada ya siku 14 kuku hurudia tena kutaga

Muhimu: Inashauriwa kutokuwa na majogoo wengi, hivyo yakupasa kudhibiti ongezeko la majogoo ndani ya banda. Waweza kufanya hivyo kwa kuhakikisha unayatambua mayai yanayoweza kuwa na mbegu ya jogoo mapema. Utafiti unaonyesha kuwa mayai membamba yenye ncha kali huwa na mbegu ya jogoo, hivyo yanaweza kuondolewa na kuliwa na familia au kuuzwa. Kwa utaratibu huo utakuwa umedhibiti ongezeko la majogoo ndani ya banda, isipokuwa kama unahitaji majogoo kwa ajii ya biashara waweza kuzalisha mengi zaidi.

Post a Comment

Previous Post Next Post